TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
- PROF.LIPUMBA KUONGOZA,MAANDAMANO KUPOKELEWA NA RAIS KIKWETE.
Waheshimiwa waandishi wa habari, kwa niaba
yangu binafsi na kwa niaba ya uongozi wote wa kitaifa wa Chama chetu,
naomba kuchukua fursa hii kuwakaribisha Ofisi Kuu ya chama ili tupate
fursa ya kuzungumza nanyi na kwa maana hiyo kuzungumza na watanzania
kupia kwenu ili ujumbe uliokusudiwa na chama uweze kuwafikia wananchi
popote pale walipo.
Tumewaita
leo tarehe 22 Juni 2013 tukiwa na agenda moja kuu nayo ni kuwaeleza
kwamba Chama cha Wananchi CUF kimeandaa Maandamano ya Amani siku ya
tarehe 29 Juni 2013 maandamano ambayo yataanzia eneo la Buguruni kituo
cha Mafuta saa nne kamili asubuhi, kupitia barabara ya Uhuru,
Mnazimmoja, Bibi Titi, Posta mpya , Aridhi hadi Ikulu.
Maandamano
hayo ambayo yataongozwa na Mwenyekiti wa Chama taifa Profesa Ibrahim
Haruna Lipumba, yanatarajiwa kupokelewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania au mwakilishi wake, na kwamba yanalengo la kufikisha
malalamiko ya wananchi kutokana na vitendo vya ukatili vinavyofanywa na
jeshi la polisi na jeshi la wananchi ambalo kimsingi taifa letu
linaelekea mahali pabaya.
Waheshimiwa waandishi wabari, mtakumbuka tarehe 15 Juni 2013 wakati
Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema wakihitimisha mkutano wa
kampeni ya uchaguzi mdogo wa udiwani katika Kata nne za Arusha,
palitokea mlipuko wa bomu uliopoteza maisha ya wananchi wane kwa mujibu
wa taarifa za polisi na wengine wengi kujeruiwa vibaya.
Kwa kuwa
jambo hili lipo katika hatua za uchunguzi, Chama cha CUF hakikusudii
kuingilia uchunguzi unaoendelea lakini tunataka kufikisha ujumbe kwa
rais kwamba hii si mara ya kwanza kuundwa kwa tume mbalimbali za
uchunguzi hapa nchini. Kinachotusikitisha ni kuwa hata mara baada ya
uchunguzi huo, hakuna ripoti inayotolewa hadharani kuonyesha chanzo cha
tukio, wahusika na hatua zilizo au zinazotarajiwa kuchukuiliwa.
Tutamtaka
Mheshimiwa rais kuhakikisha ripoti ya uchunguzi itokanayo na maafa
yaliyotokea Arusha iwekwe wazi na serikali iwachukulie hatua stahiki
wale wote watakaobainika kuhusika na tukio hilo ili iwe funzo kwa
wengine au wale wenye kuwa na malengo yanayofanana na hayo kwa kuwa
Tanzania ni yetu sote na haitowezekana watu wachache wayachezee maisha
ya watu kwa sababu ya kukidhi matakwa binafsi ambayo hayana tija kwa
jamii.
Maandamano
pia yanalenga kuishinikiza serikali kukomesha vitendo vya kinyama,
vitendo vya kijangili vinavyofanywa na Jeshi la Polisi na Jeshi la
Wananchi wa Tanzania kwa kuwakamata, kuwatesa, na kubaka wananchi wasio
na hatia wa Mkoa wa Mtwara na hasa wanaoishi katika wilaya za Mtwara
Mjini, MtwaraVijijini, na Newala huku baadhi yao wakichomewa nyumba zao
moto na wengine wakiporwa mali zao.
Waheshimiwa waandishi wa habari, mtakumbuka hivi karibuni pamekuwa na
fukuto la suala la gesi katika Mkoa wa Mtwara ambapo baadhi ya maafisa
wa Serikali wamekuwa wakipotosha madai ya wananchi ikidaiwa kwamba
wananchi wa mkoa huo wamesema hawako tayari kuona gesi yao inatumiwa na
wananchi wengine kinyume na wale wa mikoa ya Lindi na Mtwara jambo
ambalo si kweli lakini wanayafanya haya ili kuwajengea chuki dhidi ya
watanzania wengine ionekane kwamba wananchi wa Mtwara na Lindi ni
wabinafsi na wasioitakia mema nchi yetu.
Madai ya
wananchi wa Mtwara yanatokana na uzoefu waliokuwa nao katika maeneo yote
ambapo pana miradi ya kimaenedeleo itokanayo na maliasili ya nchi,
maeneo hayo yamekuwa masikini na watu wachache wamekuwa wanatajirika,
walichotaka kufahamu wananchi watanufaikaje na uwepo wa gesi katika
maeneo yao kabla ya kuinufaisha nchi mzima kwa kuwa wao ndiyo watakuwa
wa kwanza kuathirika ikiwa patatokea hitilafu yoyote itokanayo na
uchimbwaji wa gesi hiyo.
Leo
tunaweza kujifunza kutokana na uchimbaji wa Dhahabu Geita (GGM),
uchimbaji wa Almasi Mwadui Shinyanga, Mgodi wa Dhahabu wa North Mara,
Nyamongo na maeneo mengine mengi, nini hali ya maisha ya wananchi wa
maeneo hayo.
Pamoja na
upotoshwaji wa makusudi uliofanywa na unaoendelea kufanywa na watendaji
wa serikali juu ya suala la gesi ya Mtwara, inashangaza hata Jeshi la
Wananchi wa Tanzania ambalo lilionekana awali kutenda haki kwa wananchi
wa Mtwara baada ya wananchi kukosa imani dhidi ya Polisi kutokana na
wizi na uporaji wa mali za wananchi huku wakichoma moto baadhi ya maduka
kwa lengo la kuhalalisha vitendo vya hujuma pamoja na kuchoma moto soko
la Nkana Read, Jeshi lililojijengea heshima kwa jamii nalo limeanza
kuingia mkumbo wa kuwatesa raia bila makosa.
Mwanzoni
mwa wiki hii Mkurugenzi wetu wa siasa wa wilaya ya Mtwara Mjini Mhe.
Saibogi ambaye pia ni mwenyekiti wetu wa serikali ya Mtaa alitekwa na
wanajeshi na kumpeleka katika Kambi yao iliyopo barabara ya kwenda
Nanyamba ambapo walimvua nguo na kumpiga mijeredi usiku kucha bila hatia
na kumuachia asubuhi yake huku wakiahidi kuwakamata viongozi wengine wa
CUF ili kutoa funzo kwa wale wanaopigania haki za wananchi.
Matukio ya
namna hii si ya kuyafumbia macho na yanatengeneza serikali yenye kiburi
isiyotokana na maamuzi ya raia. Maisha ya namna hii hayawezi kuendeshwa
katika nchi inayojiita huru kama yakwetu na badala yake mambo haya
yanatukumbusha enzi za utawala wa kikoloni ambpo CUF kamwe hatupo tayari
kuruhusu vitendo vya kishenzi kuona vinafanyika nchini petu.
Tulikianzisha Chama hiki kwa madhumuni ya kuwaunganisha watanzania wote
popote walipo, bila kujali itikadi zao, waweze kukataa aina yoyote ya
uonevu, ukandamizaji, unyanyasaji, ubaguzi na udhalilishaji wa kisiasa
au kiuchumi.
Aidha tuna
dhamira ya kulinda, kutekeleza na kuzienzi haki za Binadamu pamoja na
kuinua uchumi wa nchi kwa siasa zitumikie uchumi badala ya uchumi
kutumikia siasa kama inavyofanyika hivi sasa. CUF tunaamini katika siasa
za ustaharabu ambazo zitatuwezesha kuwa na jamii salama yenye
mshikamano na ushirikiano katika kuijenga nchi yetu, lakini wenzetu
wanatumia upole wetu na ustaharabu wetu kutufanyia vitendo vinavyokiuka
utu wa mtu na hatimaye kila aliyepewa mamlaka ya kuongoza sehemu ya nchi
yetu anageuka kuwa mfalme na kuamrisha kamata Yule, mpe kesi Yule na
mwache Yule. Uvumilivu wetu usiwe mtaji kwa CCM na serikali yake
kutufanya watakalo, nasi ni binadamu.
Waheshimiwa waandishi wa habari, maandamano yetu yanalenga pia kuitaka
serikali kuwasikiliza wananchi wa Mtwara kwa kukaa nao chini, kujua hoja
zao na kutoa ufafanuzi pale patakapobidi, sisi tunaamini wanazo hoja za
msingi na wakisikilizwa serikali itaona namna ya kuzifanyia kazi hoja
hizo badala ya kukurupuka na kutoa kauli za kibabe eti hawa wanachochewa
na vyama vya siasa au pana watu wasioitakia mema nchi ndiyo
wanachochea, kauli hizi zinajenga chuki na zanakosa uzalendo wa taifa.
Haiwezekani hao wanaojiita ndiyo wazalendo halisi wawe wanaifidi nchi
alafu tuendelee kukaa kimya kama vile wananchi wa kusini ni watu
wasioweza kufikiri na kupambanua baya na zuri.
Wakati
wananchi hawa walipopeleka maombi yao kupitia kwa Mhe. Mohamedi Habibu
Mnyaa Mbunge wa Mkanyageni, ilikuwa nafasi nzuri kwa serikali kuweza
kusikiliza maombi yao na kutoa maamuzi, badala yake siasa zikatumika,
maombi yakakataliwa leo Bunge linaunda kamati ya uchunguzi iende mtwara
wakachunguze nini ikiwa tayari hoja zao zilikataliwa?
Ieleweke
kuwa nchi yetu itajengwa na watanzania wenyewe kwa kushirikiana na
kusikilizana. Amani ya kweli itapatikana ikiwa haki itaonekana kutendeka
kwa jamii yote. Waheshimiwa waandishi wa habari, haya ni sehemu tu ya
mambo ambayo tunakusidia kumfikishia rais wetu ili aweze kuyafanyia
kazi.
Mungu Ibariki CUF, Mungu ibarika Tanzania.
No comments:
Post a Comment